Mtazamo wa Ndani Katika Maisha ya Sanaa Kambi
Je, umewahi kujiuliza ni nini kinachohitajika ili kuunda sanaa katika mazingira magumu?
Katika mahojiano ya kipekee na Secret Of Future, mwongozaji, mwigizaji na msanii mahiri kutoka Kakuma, RACK DE OSBORN wa Tuyajenge Film Production, amefungua moyo wake na kueleza safari yake ya kusisimua. Ni safari iliyojaa mapenzi, changamoto za kambi, na maono makubwa.
Akiwa ni mmoja wa sauti zinazoibuka kwa kasi katika ulimwengu wa filamu hapa Kakuma, RACK DE OSBORN anazungumza waziwazi kuhusu namna alivyobadilisha mapenzi yake ya uigizaji na uongozaji kuwa taaluma, na kueleza kiini cha utofauti wa Tuyajenge.
Endelea kusoma ili ugundue siri za mbinu yake ya kuongoza, changamoto za vifaa, na kwa nini anatamani siku moja aweze kuonyesha hadithi yake ya maisha kwenye 'big screen' – hadithi yenye uhalisia wa kuishi kama mkimbizi. Hii ni stori inayosisimua kuhusu uvumilivu na ubunifu katikati ya Machafuko ya Kakuma.
Muhtasari na Yaliyomo Muhimu Kwenye Mahojiano
1. Kuongoza na Mapenzi Yake: Kusukuma Wasanii kwa Ukamilifu
RACK DE OSBORN anasema msukumo wake mkuu wa kufanya uongozaji ni "passion" (mapenzi) ya dhati. Anafichua kuwa siri ya kazi zake ni kuhakikisha anamsukuma msanii kufanya kile anachokipenda yeye kama muongozaji, na kukifanya kiwe "perfect."
"Nakuwa nafanya msukumo sana kwa wasanii ili kufanya kitu perfect," - RACK DE OSBORN.
Anakumbuka changamoto moja kubwa iliyomkabili, ambapo ilimbidi aingie kwenye uhusika mwenyewe na kumuonyesha mwigizaji wa kiume namna ya kuigiza kama shoga, kwani mwigizaji huyo alishindwa: "Hiyo ni scene ambayo ilinipanga challenge sana katika maisha yangu ya directive sana."
2. Ndoto ya Hadithi Yake Binafsi na Uhalisia wa Kakuma
RACK DE OSBORN anatamani sana siku moja atoe hadithi yake ya maisha, ambayo inahusiana moja kwa moja na uhalisia wa kuishi kama mkimbizi.
Anapendekeza kuwa stori zinazotakiwa kusimuliwa Kakuma ziendane na changamoto wanazopitia wakimbizi na mazingira ya kambi, ingawa anaeleza kuwa mazingira mara nyingine hayawezeshi kuelezea ukweli wote huo.
Jina la Filamu ya Kakuma: Alipoulizwa jina la filamu angaloipa Kakuma, alichagua jina la kushtua: "Machafuko." Anafafanua kuwa hili linatokana na mchanganyiko wa makabila na utaifa mwingi (nationality) kambi, na hivyo kupelekea mwingiliano wa tabia na machafuko ya tamaduni.
3. Changamoto za Uzalishaji: Vifaa na Mazingira
RACK DE OSBORN anataja vikwazo vitatu vikubwa wanavyokabiliana navyo:
Vifaa: Ukosefu wa vifaa bora huathiri ubora (quality) wa kazi wanazozalisha.
Mazingira ya Kakuma: Jua kali sana ni hali ambayo watu wa nje hawaijui, huku kelele na umati wa watu kwenye location zikiwa ni kero kubwa wakati wa shooting.
Wasanii Wagumu: Kudeal na wasanii ambao ni wagumu kuelewa kunahitaji uvumilivu na kuwapa muda wa kutulia ili pressure iishe.
4. Maono ya Tuyajenge na Ushauri kwa Wanaoanza
RACK DE OSBORN anaipenda sana Tuyajenge Film Production kwa sababu ya ushirikiano, ueledi, na viongozi wanaopenda kazi yao. Ana matumaini makubwa kuwa ndani ya miaka mitano ijayo, Tuyajenge itakuwa na uwezo wa kumtoa msanii yeyote nje ya Kakuma na kufanya naye kazi.
Ushauri wake kwa waigizaji/waongozaji wachanga: Anawatahadharisha wakae mbali na vishawishi vya mapenzi kazini, kwani anasema "hizo mara ingine huwa zinaharibu kundi na huwa zinaharibu karia yako".
Tazama Mahojiano Kamili!
Ili kumsikia RACK DE OSBORN akifunguka zaidi kuhusu kazi yake, umuhimu wa acting kwake kuliko directing, na maono yake kwa sanaa ya Kakuma, tazama mahojiano kamili hapa:
Voice Of Future With Rack De Osborn | Secret Of Future
Niandikie maoni yako! Je, una maoni gani kuhusu changamoto za 'Machafuko' alizozitaja RACK DE OSBORN? Umemuelewa vipi?