Wakati wengi wanafikiria Kambi ya Wakimbizi ya Kakuma, akili zao hujaa picha za changamoto na uhitaji. Lakini katikati ya hali hiyo, kuna vijana wachache sana wanaibuka na talanta kubwa inayovuka mipaka na kuleta matumaini. Mmoja wao ni Akay Jokey.
Katika mahojiano ya kipekee na 'Secret Of Future', Akay Jokey anafunguka kuhusu safari yake, kutoka mwanzo wake wa kujaribu kuimba mwaka 2020 hadi ndoto yake ya kusimama jukwaani New York.
Jua ni kwanini rap yake si burudani tu, bali ni sauti ya mtaa na kioo cha maisha wanayoishi.
Ndani ya Mahojiano na Rapa Akay Jokey
Akay Jokey, ambaye hujitambulisha kama A-K-A-Y Jokey, ni msanii wa Hip Hop na Gengeton ambaye anataja kuwa aligundua kipaji chake alipogundua anaweza kufuata "bit" (mlio wa muziki) vizuri katika rap kuliko aina nyingine za muziki.
Haya ndio mambo muhimu aliyozungumza kuhusu kazi yake:
Ujumbe Katika Muziki
Akay Jokey anaweka wazi kuwa muziki wake hauishii kwenye mapenzi au burudani tu, kama ilivyo kwa baadhi ya wasanii wa Kakuma. Badala yake, anasema rap yao ni sauti ya jamii.
Anatumia rap kupeleka ujumbe (message) kwa jamii kuhusu maisha yake, maisha ya wengine, na changamoto wanazopitia.
Anasisitiza kwamba wanarap "kitu yenye tunaona na tunarap kitu yenye iko kwa mtaa", kwa lengo la kufanya msikilizaji ajifunze, ajibilishe, au kupitia masimulizi yake.
Changamoto za Muziki Kambi
Kama msanii anayeishi katika kambi, anapitia changamoto za kipekee:
Pesa za Studio: Changamoto kubwa anayoipitia mara kwa mara ni upungufu wa pesa za kwenda studio kurekodi nyimbo.
Vizingiti vya Lugha: Anabainisha kuwa maproduza wengi kambini ni Wakongo, Warundi, au Wasomali, jambo linalofanya iwe vigumu kwao kuelewa kikamilifu lugha anayorap kwayo wakati wa kurekodi.
Kuvunjwa Moyo: Anawakubali wanao mfagilia, lakini pia anasema kuwa kuna wale wanaomwambia sauti yake au kazi yake "hauendi". Licha ya hayo, amejifunza kutosikiliza maneno ya wale wanaojaribu kumvunja moyo ili asigive up.
Ndoto na Ushauri kwa Vijana
Licha ya changamoto zote, Akay Jokey anamiliki ndoto kubwa:
Jukwaa la Kimataifa: Alisema kuwa angependa sana ku-perform New York ili aonekane na wasanii anaowapenda na kuwatamani kama vile Enely Chopa na Central Cee .
Ushauri wake: Anawahimiza warapa wenzake na vijana wote wasikate tamaa (don't give up). Anasema hata ukiona umefeli mara moja, jaribu mara ya pili na uendelee mbele mpaka siku moja utakapokuwa namba moja. Pia, anahimiza wasanii wa kambi kushiriki 'challenge' (mashindano ya muziki) kama njia ya kujisogeza mbele.
Mtazame mahojiano kamili hapa: Voice Of Future With Akay Jokey | Secret Of Future
Anawaomba wasikilizaji wake wote, 'anyote yenye anawchi', wamtafute kwa jina Akay Jokey kwenye majukwaa yote kama TikTok, YouTube, na Facebook na kumpa maoni na like ili kazi yake iende mbele.
Huu ni mfano hai wa talanta inayomea katika mazingira magumu na kutumia muziki kama silaha ya matumaini na sauti ya jamii.